DPP awafutia kesi ya uhaini vijana saba, washukuru kwa staili yao
DPP awafutia kesi ya uhaini vijana saba, washukuru kwa staili yao
Wakiwa na nyuso za furaha huku machozi yakiwalenga na wengine wakishindwa kujizuia na kulia kimyakimya, walinyanyua mikono juu ikiwa ni ishara ya kumshukuru muumba wao, baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwafutia kesi ya uhaini vijana saba.
Vijana hao ni waliokuwa wanakabiliwa mashtaka mawili ikiwemo kula njama na kutenda kosa la uhaini.
Sio tu, waliinua mikono juu, bali pia walipinga magoti chini na kunyanyua nyuso zao juu wakiashiria kumshukuru Mungu na kisha kutoa neno moja mbele ya Mahakama hiyo kwa kutamka “Tunamshukuru sana mheshimiwa Hakimu” huku wakimalizia kwa kukunja mikono yao na kisha kuiweka kifuani huku nyuso zao wakiziinamisha chini kuashiria kushukuru.
Hali hiyo ilijidhihirisha hata kwa mmoja wa washtakiwa, Baraka Mwita, ambaye yeye anatumia magongo mawili kutembelea, ambapo lilipofika suala la kuishukuru Mahakama, alilaza chini magongo yake naye kuungana na wenzake kwa kuinamisha kichwa chini na kuweka mikono kifuani, huku akiwa amekaa kwenye kiti kwa sababu hakuwezi kupiga magodi.
Vijana hao ni kati ya washtakiwa 95 waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya uhaini, katika kindi la sita kati ya makundi saba ya washtakiwa waliokuwa wanakabiliwa na kesi hizo katika mahakama hiyo.
Hayo yalijiri jana jioni, Desemba 24, 2025 baada ya Mahakama ya Hakimu Kisutu, kuwaachia huru washtakiwa saba wa kesi ya uhaini inayotokana na maandamano ya wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.





