Mahakama ya Rufani yaitoa Chadema kifungoni, rasmi kufanya siasa

Mahakama ya Rufani yaitoa Chadema kifungoni, rasmi kufanya siasa

Mahakama ya Rufani imekiondolea kifungo cha kutofanya shughuli za kisiasa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) baada ya kuondoa zuio hilo lililowekwa na Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam.

Uamuzi huo wa kukiweka huru chama hicho na kukiruhusu kuendelea na shughuli zake za kisiasa umetolewa na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani, Jaji Augustine Mwarija, Jaji Issa Maige na Jaji Abraham Mwampashi, leo Jumatano, Aprili 15, 2026.

Uamuzi huo umetokana na mashauri ya mapitio ya Mahakama yaliyofunguliwa na Mahakama yenyewe kutokana na kesi ya msingi ya madai ya mgawanyo usio sawa wa rasilimali za chama hicho baina ya Bara na Zanzibar.

Kesi hiyo imefunguliwa Mahakama Kuu Dar es Salaam na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chadema, Said Issa Mohamed, pamoja na wajumbe wawili wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu.

Hata hivyo, Mahakama ya Rufani, baada ya kuitisha na kusikiliza mashauri ya mapitio ya mwenendo na uamuzi mdogo wa Mahakama Kuu kuhusiana na kesi ya msingi na mashauri madogo yaliyotokana na kesi hiyo, likiwemo la zuio hilo la kufanya siasa, imetengua uamuzi huo wa zuio.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button