Mama Ahamia Kituo Cha Wazee Kumlea Mtoto Wake wa Miaka 80
Mama Ahamia Kituo Cha Wazee Kumlea Mtoto Wake wa Miaka 80.
Mwaka 2017, dunia iliguswa na simulizi ya Ada Keating, mama mwenye umri wa miaka 98 kutoka Liverpool, Uingereza, aliyefanya uamuzi wa kipekee wa kuhamia katika kituo cha kulelea wazee ili kuwa karibu na mwanae Tom, mwenye umri wa miaka 80.
Tom, ambaye alikuwa fundi rangi na mpambaji wa majengo, aliingia kwenye kituo cha Moss View Care Home mwaka 2016 kutokana na changamoto za kiafya. Mwaka uliofuata, Ada – aliyewahi kuwa muuguzi msaidizi – alijiunga naye ili kuendelea kumtunza, akisema kwa maneno yenye kugusa moyo: “Huwezi kuacha kuwa mama.”
Wawili hao walikuwa wameishi pamoja maisha yao yote, kwani Tom hakuwahi kuoa. Hata walipokuwa kituoni, waliendelea na utaratibu wao wa kila siku: kula pamoja, kutazama televisheni bega kwa bega, na kutakiana usiku mwema kabla ya kulala.
Kisa chao kilienea duniani kote, kikionekana kama mfano wa upendo wa mama kwa mwanawe hauna kikomo haupungui kwa umri, bali huimarika zaidi.






