Marekani kuziteka bandari za Iran kuanzia leo
Marekani kuziteka bandari za Iran kuanzia leo
Jeshi la Marekani limetangaza kuanza operesheni ya kuzingira bandari za Iran kuanzia leo Jumatatu Aprili 13,2026, huku likisisitiza kuwa hatua hiyo haitazuia meli zinazopita katika Mlango wa Bahari wa Hormuz kuelekea au kutoka mataifa mengine.
Kwa mujibu wa Kamandi Kuu ya Marekani, operesheni hiyo itaanza saa 10:00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki, ikihusisha ukaguzi wa meli zinazoingia na kutoka katika bandari za Iran.
Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema hatua hiyo inalenga kujibu kile alichodai ni hatua ya Iran kukataa makusudi kufungua tena Mlango wa Bahari wa Hormuz, ambao ni muhimu kwa usafirishaji wa nishati duniani.
Trump ameonya kuwa Jeshi la Wanamaji la Marekani litachukua hatua kali dhidi ya shambulio lolote kutoka Iran, akisisitiza kuwa litawaangamiza Wairan wowote watakaoshambulia, na kuongeza kuwa hatua zitachukuliwa pia dhidi ya meli zitakazolipa ushuru kwa Iran.
Aidha, Trump amesema mazungumzo yaliyofanyika mjini Islamabad, Pakistan yalishindikana kufikia muafaka, akidai kuwa Iran haipo tayari kuachana na malengo yake ya nyuklia.





