Mwanafunzi wa kiume wa kidato cha sita ampiga mwalimu wake kwa kutumia chepe kichwani na kumsababishia majeraha.
Ama kweli ukistaajabu ya Mussa, utaona ya Firauni. Ndivyo unavyoweza kusema kwa kile kinachodaiwa kuwa mwanafunzi wa kiume wa kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Mwika iliyopo Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro kumpiga mwalimu wake kwa kutumia chepe kichwani na kumsababishia majeraha.
Tukio hilo linadaiwa kutokea usiku wa Machi 25, 2024 wakati mwalimu huyo anayetambulika kwa jina moja la Matendo, alipokuwa akizunguka kukagua wanafunzi waliokuwa wanajisomea nyakati za usiku, ndipo alipovamiwa na mwanafunzi huyo na kumjeruhi kisha kutoroka shuleni hapo.
Alipotafutwa Ofisa Elimu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Jimmy Nkwamu kuzungumzia suala hilo amesema taarifa za tukio hilo alizipata na jana Machi 26, 2024 alimtuma Ofisa elimu wa wilaya hiyo kwenda kufuatilia shuleni hapo ili kujua ni nini hasa kilitokea.
“Nilimtuma jana Ofisa elimu wilaya (DEO) kwa niaba yangu aende shuleni, lakini bado hajaniletea hiyo taarifa, naomba nifuatilie, sasa hivi siwezi kuzungumza chochote juu ya tukio hilo,”amesema.






