Polisi Yaanza Msako Mtuhumiwa Anayedaiwa Kubaka, Kuua Wanawake

Polisi Yaanza Msako Mtuhumiwa Anayedaiwa Kubaka,Kuua Wanawake

Polisi katika Kaunti Ndogo ya Gem-Yala, Kaunti ya Siaya nchini Kenya, wameanzisha msako kumtafuta mtuhumiwa wa mauaji, Charles Onyango maarufu kama ‘Kwa’, anayetuhumiwa kuhusika na mauaji mfululizo yaliyotokea eneo hilo kwa miezi kadhaa sasa.

Kamanda wa Polisi wa Gem, Charles Wafula amesema mtuhumiwa huyo amekuwa tishio kwa usalama wa wakazi, hasa wanawake na wasichana wadogo, ambao wamekuwa waathirika wa mashambulizi hayo yenye taswira ya ukatili.

“Mtuhumiwa huyu huwa anawanyanyasa kingono waathirika hao kabla ya kuwaua. Ni hali ya kusikitisha na tunafanya kila jitihada kuhakikisha anapatikana,” amesema Kamanda Wafula.

Amesema msako dhidi ya Onyango unaendelea kwa juhudi zote na tayari vikosi maalumu vya usalama vimepelekwa katika maeneo mbalimbali anapodhaniwa kujificha.

“Tunaendelea kufuatilia taarifa zozote zinazoweza kutufikisha alipo. Tunawaomba wananchi watoe ushirikiano kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwake,” amesema Wafula.

Matukio hayo ya mauaji yamezua hofu kubwa miongoni mwa wakazi wa Gem-Yala, huku wengi wakieleza wasiwasi wa usalama wao na wa familia zao, hasa watoto wa kike. Wakazi wameitaka Serikali kuchukua hatua za haraka ili kumaliza jinai hizo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button