Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete ameongoza ujumbe wa Wajumbe wa Bodi kutoka Afrika wa Shirika la Kimataifa la Lishe
Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete ameongoza ujumbe wa Wajumbe wa Bodi kutoka Afrika wa Shirika la Kimataifa la Lishe (Nutrition International, NI) kukutana na Spika wa Bunge la Kanada Gregory Fergus katika Ofisi za Bunge la nchi hiyo zilizopo Ottawa, Kanada. Kikao hicho kimehudhuriwa pia wajumbe wengine wa Bodi hiyo ambao ni Dkt. Ibrahim Mayaki, Waziri Mkuu Mstaafu wa Niger na Bi. vivianonano kutoka Kenya.
Dkt. Kikwete na ujumbe alioambata nao walitumia fursa ya kikao hicho kueleza kwa undani kazi kubwa zinazofanywa na Shirika hilo la Kimataifa la Lishe lenye makao makuu nchini Kanada katika kupambana na tatizo la utapiamlo duniani, hususan katika nchi zinazoendelea zikiwemo za bara la Afrika.
Aidha, kupitia kikao hicho kilichohudhuriwa pia na wajumbe wa Kamati mbalimbali za Bunge hilo, Dkt. Kikwete aliishukuru Kanada kwa kuendelea kufadhili kazi za Shirika hilo la NI kwa zaidi ya miaka 30 ambapo kupitia kazi zake takriban maisha milioni 34 ya watoto wachanga, watoto wenye umri chini ya miaka mitano, wasichana balehe na wanawake wajawazito yameokolewa duniani kote, hususan katika nchi za bara la Asia na Afrika.
Kwa upande wake Spika Fergus alimshukuru Dkt. Kikwete na ujumbe alioambatana nao kwa kutambua umuhimu wa kulishirikisha Bunge la Kanada katika kazi kubwa inayofanywa na Shirika hilo lisilo la kiserikali. Akamweleza anatambua kuwa lishe bora ni moja ya haki za msingi za kila mwanadamu na kwamba Kanada itaendelea kuwa nchi kinara katika kufadhili miradi mbalimbali inayolenga kuboresha upatikanaji wa lishe bora na virutubisho duniani.
Shirika hilo lenye Ofisi katika nchi tano za Afrika zikiwemo Tanzania, Ethiopia, Kenya, Nigeria na Senegal limejikita katika kutoa lishe nyongeza zilizothibitishwa kitaalamu, zenye ufanisi wa hali ya juu na zinazopatikana kwa gharama nafuu. Kupitia programu kama vile urutubishaji wa nafaka na mafuta ya kula, na uwekaji wa madini ya joto kwenye chumvi (iodini), Shirika hilo la la NI linasaidia jitihada za Serikali za nchi zinazoendelea kukabiliana na tatizo la udumavu na unyafuzi kwa watoto, yaani watoto kuwa na urefu au uzito mdogo zaidi kulingana na umri wao.







