RAISI SAMIA APANGUWA BARAZA LA MAWAZIRI NA MAKATIBU WAKUU

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri na Makatibu Wakuu ambapo amemhamisha January Makamba kutoka Wizara ya Nishati kwenda kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Pia amemteua Mbunge wa Ukonga Jerry Silaa kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, awali Wizara hiyo ilikuwa ikiongozwa na Waziri Angelina Mabula ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

Rais Samia amemteua Anthony Mavunde kuwa Waziri wa Madini, ambapo Kabla ya uteuzi huo, Mavunde alikuwa Naibu Waziri wa Kilimo.

Profesa Makame Mbarawa yeye ameteuliwa kuwa Waziri wa Uchukuzi, Kabla ya uteuzi huo, Mbarawa alikuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi huku Innocent Bashungwa aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ameteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi.

Aidha Rais Samia amemuhamisha Damas Ndumbaro kutoka Wizara ya Katiba na Sheria kwenda kuwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, pia amemuhamisha Angellah Kairuki kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI kwenda kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii.

Hata hivyo Rais Samia amemteua Doto Biteko kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati.

Imeelezwa kuwa katika nafasi ya Naibu Waziri Mkuu Biteko atakuwa anashughulikia utaratibu wa shughuli za Serikali.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Dk. Moses Kusiluka imeeleza kuwa uteuzi huo unaanza leo Agosti 30, 2023 na kwamba viongozi walioteuliwa wataapishwa Septemba Mosi, 2023 Ikulu Ndogo Zanzibar saa 5:00 asubuhi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button