Ruto aitisha mkutano wa dharura EAC, sababu yatajwa

Ruto aitisha mkutano wa dharura EAC, sababu yatajwa

Rais wa Kenya, William Ruto, ameita mkutanowa dharura wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) utakaofanyika Machi 7, 2026 jijini Arusha, kujadili mgogoro mkubwa wa kifedha unaotikisa jumuiya hiyo ya kikanda.

Mkutano huo, utakaokuwa wa kwanza kufanyika baada ya zaidi ya mwaka mmoja, unatarajiwa kujadili mfumo mpya wa uchangiaji wa fedha na hatua za kupunguza matumizi ndani ya EAC, baada ya nchi wanachama kushindwa kuwasilisha zaidi ya Dola 89.3 milioni (Sh232.78 bilioni) zinazodaiwa na taasisi za jumuiya hiyo.

Rais Ruto, ambaye ni Mwenyekiti wa Wakuu wa Nchi wa EAC, anatarajia marais wote wanane wa nchi wanachama kushiriki, huku akisisitiza kuwa uamuzi wa mwisho kuhusu mgogoro huo uko mikononi mwa viongozi hao.

Waziri wa Kenya anayeshughulikia Masuala ya EAC, Mikoa Kame na Maendeleo ya Kanda, Beatrice Askul, amesema mkutano huo utashughulikia uhaba wa fedha, kupitisha mfumo mpya wa ufadhili uliopendekezwa na Baraza la Mawaziri la EAC, na kukubaliana namna ya kuratibu matumizi.

“Rais wa Kenya ambaye ndiye mwenyekiti wa mkutano wa wakuu wa nchi ana nia ya dhati kuona viongozi wanatoa msimamo wao kuhusu suala hili, kwa sababu wao ndiyo chombo cha mwisho cha maamuzi ndani ya EAC,” amesema Askul.

Taarifa zinaonyesha kuwa hadi Januari 31, 2026, EAC ilikuwa inaidai nchi wanachama dola 89,372,865, huku Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ikiongoza kwa deni la dola milioni 27, ikifuatiwa na Burundi (dola milioni 22.7), Sudan Kusini (dola milioni 21.8), Somalia (dola milioni 10.5), Rwanda (dola milioni 5.2) na Uganda (dola milioni 1.1). Kenya na Tanzania pekee ndizo zilikuwa zimelipa kikamilifu mchango wa dola milioni saba kwa mwaka wa fedha 2025/26.

Ukosefu huo wa fedha umeathiri kwa kiasi kikubwa uendeshaji wa taasisi muhimu za EAC, zikiwamo Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Mahakama ya Afrika Mashariki na taasisi nyingine In za kikanda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button