Serikali, wadau, mguu sawa ujenzi wa viwanda vya dawa Tanzania
Serikali, wadau, mguu sawa ujenzi wa viwanda vya dawa Tanzania
Serikali imetangaza mkakati mpana wa kuharakisha uwekezaji katika uzalishaji wa dawa, ikilenga kuiweka nchi kama kitovu cha kikanda na Bara la Afrika katika uzalishaji wa dawa zenye viwango vya kimataifa.
Hatua hiyo imekuja sambamba na ahadi ya ulinzi wa soko kwa wazalishaji wa ndani watakaokidhi viwango vya Shirika la Afya Duniani (WHO).
Inaelezwa awali kuwa changamoto kubwa iliyokwamisha viwanda vya ndani vya dawa ilikuwa ni kushindwa kufikia viwango vya kimataifa vya uzalishaji, hususan vinavyotambuliwa na WHO na Good Manufacturing Practice (GMP).
Akizungumza leo Jumatatu, Januari 19, 2026, katika Jukwaa la Kimkakati la Uwekezaji wa Bidhaa za Afya Tanzania, Waziri wa Afya, Mohammed Mchengerwa, amesema Serikali imeamua kuondoa utegemezi mkubwa wa dawa zinazoagizwa kutoka nje, akisisitiza kuwa usalama wa afya ya taifa hauwezi kujengwa kwa uagizaji pekee.
Amesema Serikali imeanzisha Mkakati wa Kuharakisha Sekta ya Dawa (Pharmaceutical Acceleration Strategy) unaolenga kuondoa urasimu na kucheleweshwa kwa maamuzi ya uwekezaji.





