Trump: Marekani haitaondoa kizuizi cha kijeshi Hormuz hadi makubaliano na Iran yafikiwe

Trump: Marekani haitaondoa kizuizi cha kijeshi Hormuz hadi makubaliano na Iran yafikiwe

Rais wa Marekani, Donald Trump amesema nchi hiyo haitaondoa kizuizi cha kijeshi ilichoweka katika maeneo ya bahari ya Mlango wa Hormuz hadi pale makubaliano rasmi yatakapofikiwa na Iran.

Kauli hiyo imekuja wakati kukiwa na sintofahamu juu ya mustakabali wa mazungumzo ya amani kati ya Marekani na Iran, huku pande hizo zikionesha msimamo tofauti kuhusu hatua inayofuata.

Kupitia mtandao wake wa Truth Social, Trump amesema kizuizi hicho, kilichoanza wiki moja iliyopita, kinaidhoofisha kabisa Iran, akisisitiza kuwa Marekani inaendelea kushinda mzozo huo kwa kiwango kikubwa.

Hata hivyo, kauli ya Trump imekuja sambamba na taarifa za kuwepo kwa makubaliano ya muda ya kusitisha mapigano kati ya pande hizo mbili, yanayotarajiwa kukamilika kesho Jumatano, ingawa hatima ya mazungumzo ya awamu ya pili bado haijawa wazi.

Ripoti zinaeleza kuwa mkutano wa mazungumzo hayo unatarajiwa kufanyika nchini Pakistan, ambako hali ya usalama imeimarishwa katika mji mkuu kwa ajili ya tukio hilo.

Kwa upande wa Marekani, Makamu wa Rais JD Vance anatarajiwa kuongoza ujumbe wa nchi hiyo, lakini hadi sasa hajaanza safari kutoka Washington. Wakati huo huo, Iran imesema bado haijatoa uamuzi wa kushiriki mazungumzo hayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button