Trump: Nchi itakayofanya biashara na Iran italipa ushuru wa asilimia 25
Trump: Nchi itakayofanya biashara na Iran italipa ushuru wa asilimia 25
Rais wa Marekani, Donald Trump ametoa onyo kali kwa mataifa yote yanayofanya biashara na Iran, akitangaza kuwa nchi yoyote itakayoendelea kushirikiana kibiashara itakabiliwa na ushuru mpya wa asilimia 25 kwa bidhaa zake zote zinazoingia katika soko la Marekani.
Hatua hiyo imekuja wakati utawala wa Trump ukiendelea kuishinikiza Iran kusitisha kile kinachoelezwa kuwa ukandamizaji wa waandamanaji wanaopinga Serikali ya kidini nchini humo.
“Kuanzia hivi sasa nchi yoyote inayofanya biashara na Iran italazimika kulipa ushuru wa asilimia 25 kwa biashara zote inazofanya na Marekani,” Trump amesema katika chapisho lake kwenye mtandao wa Truth Social.
Kupitia chapisho hilo, Trump amesema agizo hilo ni la mwisho, akiongeza shinikizo la kiuchumi sambamba na vitisho vya awali vya kuchukua hatua za kijeshi.
“Agizo hili ni la mwisho na la hitimisho,” amesema Trump, akibainisha kuwa lengo ni kudhoofisha uchumi wa Iran unaotegemea kwa kiasi kikubwa mauzo ya mafuta. Iran huuza mafuta yake kwa nchi kadhaa zikiwemo China, Uturuki, Iraq, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na India.
Ubalozi wa China mjini Washington umeikosoa vikali kauli hiyo ya Trump, ukisema Beijing itachukua hatua zote muhimu kulinda maslahi yake ya kiuchumi.





