USA -MAFURIKO YANAVYOITESA NEW YORK CITY
Mvua kubwa isiyokuwa ya kawaida imekikumba Jiji la New York, Marekani, na kusababisha mafuriko makubwa yaliyosababisha usumbufu mkubwa wa usafiri, uharibifu wa miundombinu, na hatimaye serikali kutangaza hali ya hatari katika maeneo mbalimbali ya jiji.
Mvua hizo zilinyesha kwa kasi ya hadi inchi tatu kwa saa, huku maeneo mengi yakipokea jumla ya hadi inchi nane za mvua ndani ya saa chache tu.
Mafuriko hayo yameleta athari kubwa kwa mfumo wa reli ya chini ya ardhi (Subway), ambapo stesheni kadhaa ziliingiliwa na maji.
Abiria walilazimika kuondolewa haraka huku video zikionyesha maji yakitiririka ndani kama maporomoko ya maji.
Stesheni zilizoathirika zaidi ni pamoja na Grand Central, Jay Street-MetroTech, na Seventh Avenue huko Brooklyn.
Katika sehemu mbalimbali kama Clearview Expressway, barabara zilifunikwa kabisa na maji, magari yakielea, na baadhi ya watu kunaswa ndani ya magari yao.
Vikosi vya uokoaji vilifanikiwa kuwaokoa watu waliokuwa wamekwama.
Maelfu ya safari za ndege ziliahirishwa au kufutwa katika viwanja vya ndege vya JFK, LaGuardia, na Newark kufuatia mafuriko hayo






