Waziri Kombo apokea na kuanzisha Kifimbo cha Mbio za Mfalme wa Uingereza
Katika Viwanja vya Michezo vya Jakaya Mrisho Kikwete, Kidongo Chekundu, Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) amepokea Kifimbo cha Mfalme wa Uingereza kikitokea nchini Cameroon ikiwa ni ishara ya kuelekea kuanza kwa michezo ya Jumuiya ya Madola itakayofanyika jijini Glasgow, Scotland mwaka 2026.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyoandaliwa na Kamati ya Olimpiki Tanzania, Mhe. Kombo ameeleza kuwa kifimbo hicho si ishara ya kuanza kwa michezo hiyo maarufu duniani tu, bali ni ishara ya umoja, upekee, urafiki, maendeleo na ushirikiano wa Jumuiya ya Madola.
Aidha, Mhe. Kombo ameelezea kufurahishwa na kifimbo hicho kutumia mbao na si plastiki kama ilivyokuwa awali ikiwa ni ishara nzuri ya utunzaji wa mazingira.
Naye Naibu Balozi wa Uingereza nchini, Bi. Sally Hedley ameeleza kuwa Uingereza inaendeleza jitihada za kupambana na taka za plastiki na kuisifu Tanzania kwa kuwa mfano wa kuigwa katika utunzaji wa mazingira. Vilevile, ameeleza kuwa vifimbo vyote 74 vina sehemu ya maneno ya ujumbe wa Mfalme Charles III ambao utasomeka pindi vifimbo vyote vitakapounganishwa kwenye kilele cha mashindano ya Jumuiya hiyo mwakani.
Kadhalika, mara baada ya kuanzishwa na Mhe. Kombo, kifimbo hicho kilitembezwa toka Uwanja wa Michezo wa Jakaya Mrisho Kikwete kikipita barabara za Nkrumah, Samora hadi Makumbusho ya Taifa na kisha kupelekwa Ikulu ya Magogoni na kupokelewa na Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa niaba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hasaan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Tofauti na miaka ya nyuma, nchi zote 74 wanachama wa Jumuiya ya Madola zimepewa kifimbo cha mbao ili kila nchi iweze kukichora kwa michoro ya tamadumi zao ambapo vifimbo hivyo vitawasilishwa vyote kwenye kilele michezo hiyo Julai 2026 jijini Glasgow, Scotland.






