Ahukumiwa Miaka 6 Jela Mapenzi Ya Jinsia Moja Senegal
Ahukumiwa Miaka 6 Jela Mapenzi Ya Jinsia Moja Senegal
Mahakama moja Nchini Senegal imetoa hukumu ya kwanza chini ya sheria mpya inayoongeza adhabu dhidi ya mapenzi ya jinsia moja, ambapo Kijana mwenye umri wa miaka 24 amehukumiwa kifungo cha miaka sita jela pamoja na faini ya takribani dola za Marekani 3,300, sawa na zaidi ya milion 8.4 za Kitanzania.
Hukumu hiyo imetolewa na Mahakama iliyopo katika eneo la Pikine Guediawaye, Jijini Dakar, kufuatia Mtuhumiwa kutiwa hatiani kwa kosa lililotajwa kama vitendo vinavyokiuka maadili ya umma, Kijana huyo alikamatwa mapema mwezi huu kabla ya kufikishwa Mahakamani.
Sheria mpya iliyopitishwa hivi karibuni Nchini humo na Rais Bassirou Diomaye Faye, imeongeza adhabu kwa makosa yanayohusiana na mapenzi ya jinsia moja, ambapo sasa kifungo kinaweza kufikia kati ya miaka mitano hadi kumi Jela, mbali na hilo, sheria hiyo pia inalenga kudhibiti kile kinachoelezwa kama “kukuza” au “kufadhili” vitendo hivyo, hatua inayotafsiriwa na Wachambuzi kama njia ya kuweka vikwazo kwa makundi yanayotoa msaada kwa Watu wa jamii za wachache wanaofanya vitendo hivyo.
Hatua hiyo inaifanya Senegal kuwa miongoni mwa Nchi Barani Afrika zilizoimarisha adhabu kali zaidi katika masuala yanayohusiana na mapenzi ya jinsia moja, jambo linaloendelea kuzua mjadala mpana kuhusu haki za binadamu na uhuru wa kijamii.





