KOFFI OLOMIDE KUUNGANA NA AFRIGO BAND KATIKA MAADHIMISHO YA MIAKA 50 YA BENDI HIYO NCHINI UGANDA.

Msanii maarufu wa muziki kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Koffi Olomidé, amewasili Nchini Uganda kwa ajili ya kushiriki katika tamasha maalum la Legends of Sound: Afrigo@50, linaloadhimisha miaka 50 ya bendi ya Afrigo Band, ambayo ni bendi kongwe na maarufu zaidi Nchini Uganda.
Tamasha hili litafanyika Jumamosi, tarehe 16 Agosti 2025, katika Viwanja vya Millennium Grounds vilivyoko Lugogo, Kampala.
Afrigo Band, iliyoanzishwa mwaka 1975 na Msanii Moses Matovu, imekuwa nguzo muhimu katika tasnia ya muziki wa Uganda, ikijulikana kwa mchanganyiko wa muziki wa jadi na wa kisasa, na imeendelea kuwavutia mashabiki wa rika zote kwa miongo mitano.
Tamasha hili limeandaliwa na Talent Africa Group kwa ushirikiano na Stanbic Bank Uganda, kupitia jukwaa lao la malipo ya kidijitali la FlexiPay, ambalo pia ni mshirika rasmi wa tiketi za tamasha hilo.
Katika tamasha hilo, mashabiki watapata fursa ya kushuhudia maonyesho ya moja kwa moja kutoka kwa Wanachama wa Afrigo Band, wakiwemo Moses Matovu, Rachel Magoola, Joanita Kawalya, Herbert Kigundu, Sarah Namulondo, na Charles Busuulwa.
Koffi Olomidé, anayejulikana kwa mtindo wake wa muziki wa Ndombolo, atapamba jukwaa hilo kwa nyimbo zake maarufu kama “Ndombolo”, “Andrada”, “Cle Boa”, na “Selfie (Ekoti Te)”, akichanganya ladha ya muziki wa Congo na ule wa Uganda katika usiku huo wa kipekee.
Kwa mujibu wa Aly Allibhai, Mkurugenzi Mtendaji wa Talent Africa Group, tamasha hili ni sehemu ya mfululizo wa matamasha ya Legends of Sound, yanayolenga kusherehekea Wasanii wa muziki wa Kiafrika waliotoa mchango mkubwa katika tasnia hiyo.
Kwa mashabiki wa muziki wa Afrika Mashariki na Kati, tamasha hili ni fursa ya kipekee kushuhudia historia ya muziki ikitengenezwa, huku bendi ya Afrigo ikitimiza nusu karne ya mafanikio katika muziki.
Tiketi za tamasha zinapatikana kupitia jukwaa la FlexiPay, kwa kutumia programu ya simu au kwa kupiga *291#.
Usikose kuwa sehemu ya historia hii ya muziki wa Afrika

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button