Marekani yamwekea vikwazo Mafwele kwa tuhuma za ukiukwaji wa haki za binadamu

Marekani yamwekea vikwazo Mafwele kwa tuhuma za ukiukwaji wa haki za binadamu

Marekani imemwekea vikwazo Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Tanzania, Faustine Mafwele kwa madai ya kuhusika katika ukiukwaji wa haki za binadamu, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania.

Katika taarifa hiyo iliyotolewa Mei 21, 2026, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio amesema hatua hiyo imechukuliwa chini ya kifungu cha 7031(c) baada ya kuwepo kwa “taarifa zinazoaminika” zinazomhusisha Mafwele na vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu.

Marekani imedai kuwa baadhi ya askari wa Jeshi la Polisi Tanzania waliwakamata, kuwatesa na kuwafanyia ukatili wa kingono mwanaharakati wa Uganda, Agather Atuhaire pamoja na mwanaharakati wa Kenya, Boniface Mwangi, walipokuwa jijini Dar es Salaam kufuatilia kesi ya uhaini inayomkabili kiongozi wa upinzani, Tundu Lissu.

Tukio hilo lilizua wasiwasi mkubwa kutoka kwa mashirika ya haki za binadamu ya kikanda na kimataifa, yaliyotaka kufanyika kwa uchunguzi huru kuhusu madai ya ukiukwaji huo yaliyodaiwa kufanywa na vyombo vya usalama vya Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, vikwazo hivyo vinamzuia Mafwele kuingia nchini Marekani na vinalenga kuhimiza uwajibikaji kwa wanaohusika na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button