Ripoti Yataja Chanzo Cha Kifo Cha Rosemary Kimwatu
Ripoti Yataja Chanzo Cha Kifo Cha Rosemary Kimwatu
Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi wa Data katika Benki ya KCB Group, Rosemary Chemutai Kimwatu, amekutwa amefariki dunia nyumbani kwake eneo la Ngong nchini Kenya mnamo Agosti 21, 2026.
Ripoti ya uchunguzi wa mwili (autopsy) iliyoongozwa na Mpasuaji Mkuu wa Serikali, Dk. Johansen Oduor, imebaini kuwa chanzo cha kifo chake ni kujiua, huku polisi wakithibitisha kutokuta ujumbe wowote wa kuaga eneo la tukio.
Taarifa za awali katika mitandao ya kijamii zilihusisha tukio hilo na msongo wa mawazo uliotokana na kazi, lakini maelezo ya familia kwa jeshi la polisi yamebainisha kuwa marehemu alikuwa akipitia changamoto binafsi za kifamilia na shinikizo la madeni.
Uchunguzi zaidi unaendelea ili kubaini undani wa mazingira yaliyopelekea tukio hilo. Enzi za uhai wake, Rosemary alikuwa mtaalamu mbobezi aliyetambulika katika masuala ya sheria, teknolojia, na sera za kidijitali kote nchini humo.
Kabla ya kujiunga na nafasi yake ya uongozi ndani ya KCB, aliwahi kuhudumu kama Meneja wa Sera za Umma katika kampuni ya mawasiliano ya Safaricom pamoja na kuwa mjumbe wa bodi ya KICTANet.





