WAANDAENI WANAFUNZI VYEMA WAWEZE KUSHIRIKI UCHUMI WA KISASA – MAULID

Mkurugenzi wa Elimu Msingi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Bw. Abdul Maulid aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, ametoa wito kwa walimu wa kujitolea wa somo la Elimu ya Biashara Shule za Sekondari za Tanzania Bara kuwaandaa wanafunzi vyema ili wawe na uwezo wa kujiajiri au kuajiriwa pindi wamalizapo elimu.

Ametoa wito huo leo Agosti 10, 2026 wakati akifungua mafunzo ya siku 12 kwa walimu wakujitolea wa somo la Elimu ya Biashara katika ukumbi wa Maktaba wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

“Walimu wenzangu, jukumu lenu halitaishia kwenye kufika shuleni na kuwafundisha wanafunzi katika vituo mtakavyopangiwa tu, bali mna mambo mengine mengi ya kuyafanya kama vile kufundisha, kulea na kuhamasisha wanafunzi kujifunza, pamoja na kutumia maarifa na mbinu mtakazozipata hapa kuboresha eneo la ufundishaji na ujifunzaji,” amesema Bw. Maulid.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dkt. Fika Mwakabungu, amesema mafunzo hayo, yatawajengea washiriki umahiri wa kutekeleza Mtaala wa Elimu ya Biashara kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne.

“Ndugu walimu, mafunzo haya ni hatua muhimu sana ya kuwaandaa nyinyi ili muweze kutekeleza Mtaala kwa uelewa, weledi na ufanisi unaotarajiwa, na hatimaye kupata wanafunzi wenye uelewa kuhusu biashara na namna ya kujiajiri na kuweza kuajiriwa,” amesema Dkt. Mwakabungu.

Naye Mwakilishi wa EDUCATE, Bw. Nelson Musikula, amesema shirika lao litaendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha elimu nchini hasa kupitia somo la Elimu ya Biashara ili kukabiliana na changamoto ya ajira nchini.

Walimu hao wanafundishwa na wakufunzi mbalimbali kutoka vyuo vya ualimu pamoja na wataalamu kutoka TET, ambapo zaidi wa walimu 400 kutoka mikoa 11 nchini wanatarajiwa kupatiwa mafunzo hayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button