Sheikh Walid, wenzake waundiwa tume ya uchunguzi

Sheikh Walid, wenzake waundiwa tume ya uchunguzi

Hatimaye Baraza la Ulamaa la Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) limeunda tume ya watu sita kuchunguza tuhuma zinazowakabili masheikh watatu waliosimamishwa kwa madai ya kuwa na mwenendo unaokiuka misingi ya uongozi wa baraza hilo.

Masheikh hao ni Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Walid Alhad Omar, Sheikh wa Mkoa wa Singida, Sheikh Issa Nassor Issa, na Sheikh wa Mkoa wa Kigoma, Sheikh Hassan Idi Kiburwa. Masheikh hao walisimamishwa Julai 14, 2026, kufuatia kikao cha dharura cha Baraza la Ulamaa.

Tume hiyo imepewa jukumu la kufanya uchunguzi wa kina ndani ya kipindi cha mwezi mmoja kabla ya kuwasilisha taarifa yake kwa Mufti wa Tanzania, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Ulamaa, Sheikh Abubakar Zuber Bin Ali.

Wajumbe wanaounda tume hiyo inayotajwa inaenda kutafuta haki ni Sheikh Shaban Juma Abdallah, Sheikh wa Mkoa wa Arusha, ambaye ndiye Mwenyekiti wa tume; Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Mussa Hans; Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro, Dk Abdallah Tego; Wakili Ummi Azizi Kheri; Mkurugenzi wa Elimu Bakwata, Mwalimu Ally Abdallah; na Hamis Kalimwage, ambaye ni mjumbe wa kamati ya utatuzi wa migogoro ya misikiti na madrasa nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kikao cha Baraza la Ulamaa kilichofanyika leo, Julai 21, 2026, Katibu wa Baraza hilo, Sheikh Hassan Saidi Chizenga, amesema uamuzi wa kuunda tume hiyo ulifikiwa katika kikao kilichoongozwa na Mufti wa Tanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button