Balozi aeleza ‘unga’ unavyowagharimu Watanzania China

Balozi aeleza 'unga' unavyowagharimu Watanzania China

Balozi wa Tanzania nchini China, Dk Suleiman Haji Suleiman amesema dawa za kulevya zinaendelea kuwagharimu Watanzania wanaokwenda China, akieleza kuwa baadhi yao wamehukumiwa vifungo vya miongo kadhaa huku familia zao nchini zikipoteza mawasiliano nao na kuamini wamefariki dunia.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (Tiseza), jijini Dar es Salaam, leo Julai 14, 2026, Dk Suleiman amesema ubalozi umekutana na visa vingi vya Watanzania waliokamatwa kwa makosa ya dawa za kulevya na sasa wanatumikia adhabu katika magereza ya China kutokana na ukali wa sheria za nchi hiyo.

Ametoa mfano wa mama mmoja aliyefika kwenye banda la Ubalozi wa Tanzania wakati wa Maonesho ya Sabasaba akieleza kuwa aliarifiwa mwanaye aliyekuwa China amefariki akiwa gerezani.

“Baada ya kuchukua taarifa zake na kuzifuatilia, tulibaini kijana huyo yupo hai na anaendelea kutumikia kifungo chake. Anatarajiwa kumaliza adhabu mwaka 2031,” amesema.

Ameongeza kuwa wanawake wanaonekana kwa wingi kuwa miongoni mwa Watanzania wanaokamatwa kwa makosa hayo, akieleza kuwa wengi huingia kwenye mtandao huo baada ya kuanza safari za kawaida za biashara.

Ameonya kuwa sheria za China dhidi ya dawa za kulevya ni kali na hazitoi nafasi kwa anayebainika kufanya kosa hilo, hivyo amewasihi Watanzania wanaokwenda nchini humo kuwa waangalifu na kutokubali kubeba mizigo wasiyoifahamu kwa ahadi za kupata fedha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button