MAKONDA: ZAIDI YA WANANCHI 3,000 WAMEHUDUMIWA SIKU YA KWANZA, AIPONGEZA SERIKALI YA RAIS SAMIA NA WADAU WA AFYA

Mbunge wa Arusha Mjini na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Christian Makonda (Mb), ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Wizara ya Afya, taasisi za afya na hospitali binafsi kwa kushirikiana kufanikisha Kambi ya Matibabu Bila Malipo inayoendelea jijini Arusha.

Akizungumza baada ya kutembelea mabanda mbalimbali ya huduma za afya, Mhe. Makonda amesema mafanikio ya kambi hiyo yametokana na ushirikiano mkubwa wa Serikali na wadau wa sekta ya afya walioungana kuwasogezea wananchi huduma za kibingwa.

Amesema kwa mujibu wa taarifa za siku ya kwanza, zaidi ya wananchi 3,000 walipatiwa huduma za uchunguzi na matibabu, huku akieleza kuwa mwitikio unaendelea kuongezeka siku hadi siku.

“Mafanikio haya yasingewezekana bila ushirikiano wa Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Wizara ya Afya, taasisi zake na hospitali binafsi. Nawashukuru sana kwa kuendelea kuwahudumia wananchi wa Arusha na Watanzania kwa ujumla,” amesema Makonda.

Ameongeza kuwa katika kambi hiyo wapo madaktari bingwa kutoka taasisi mbalimbali za Serikali ikiwemo JKCI, Muhimbili, Benjamin Mkapa Hospital, Ocean Road, Mount Meru Hospital na hospitali nyingine nyingi, sambamba na hospitali binafsi zinazotoa huduma za kibingwa.

Makonda amesema lengo la kambi hiyo ni kuwafikia wananchi wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za matibabu, ili wapate uchunguzi wa mapema, matibabu na ushauri wa kitaalamu bila malipo.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button