Barcelona Yakaribia Kuvunja Rekodi Yake ya Kihistoria ya Mabao La Liga
Barcelona Yakaribia Kuvunja Rekodi Yake ya Kihistoria ya Mabao La Liga
FC Barcelona inaendelea kuthibitisha ubora wake katika msimu wa La Liga 2025/26 baada ya ushindi wa mabao 2-0 walioupata wikiendi hii, ushindi uliowawezesha kufikisha jumla ya mabao 100 katika ligi hiyo. Hatua hiyo imewafanya kuwa klabu ya kwanza kufikia idadi hiyo ya mabao kwa mara nyingine tena tangu walipofanya hivyo mwaka 2018.
Mara ya mwisho Barcelona ilivuka kizingiti cha mabao 100 ilikuwa chini ya uongozi wa nahodha wao wa wakati huo, Lionel Messi, ambapo walimaliza msimu wakiwa wamefunga mabao 102. Mafanikio ya sasa yanaonyesha wazi kuwa kikosi cha sasa kinaendelea kuandika historia yake mpya.
Safu ya ushambuliaji inayoundwa na Lamine Yamal, Raphinha na Robert Lewandowski imekuwa tishio kubwa kwa wapinzani, huku ikipelekea timu hiyo kubakiwa na mabao matatu pekee ili kuvunja rekodi ya kihistoria iliyowekwa na Messi, Luis Suárez na Ousmane Dembélé.
Kwa sasa, Barcelona imesalia na michezo miwili pekee ndani ya mwaka huu. Mchezo wa kwanza ni wa Copa del Rey watakapokabiliana na Guadalajara, kabla ya kuhitimisha mwaka kwa mchezo wa La Liga dhidi ya Villarreal ugenini tarehe 21 Disemba.
Swali kubwa kwa mashabiki na wachambuzi wa soka ni moja:-
Je, Barcelona itafanikiwa kuivunja rekodi yao ya kihistoria ya mabao kabla ya mwaka 2025 kuisha?
Macho yote sasa yanaelekezwa kwenye kikosi cha Blaugrana kusubiri jibu hilo.





