Chadema Yakomalia Hoja Yake Ya Kuahirisha Uchaguzi Mkuu 2025
Chadema Yakomalia Hoja Yake Ya Kuahirisha Uchaguzi Mkuu 2025
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),Tundu Lissu amesema kususia kila jambo watakaloletewa na Serikali ni moja ya njia ya kushinikiza kupatikana mifumo huru ya uchaguzi itakayotoa haki kwa wananchi kupata viongozi wanaowataka.
Amesema ili wafanikiwe azma hiyo ni lazima kila mmoja wao ashiriki harakati hizo huku akisisitiza kuzunguka nchi nzima kufīkisha ujumbe kwa kila Mtanzania, ingawa haitakuwa rahisi lakini anaamini wakiwa wamoja wanaweza kuvuka.
Lissu amezungumza hayo leo Machi 26,2025 kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Sumbawanga Mjini, mkoani Rukwa kwenye mwendelezo wa kampeni ya kutoa elimu kwa wananchi juu ya kampeni ya ‘No reforms no Election’ inayolenga kuishinikiza Serikali kubadili mifumo huru ya uchaguzi.
“Chochote wanachopendekeza tukisusie, kila watakachotuletea tukikatae na nimeangalia sheria za nchi sijaona sehemu kama tukikataa kwenda kupiga kura ni dhambi au tumevunja sheria, lakini ukweli wa Mungu ni kwamba hata kwa Katiba hii inawezekana kuahirishabuchaguzi,”amesema
Amesema Katiba imesema kama kuna dharura uchaguzi unaweza kuahirishwa kwa mwaka mmoja hata kama Bunge litakuwa limevunjwa likisubiri uchaguzi, ikitokea dharura Katiba inasema Bunge litaitishwa wabunge walewale kwenda kujadili dharura iliyojitokeza.