Familia Yashukuru Waliomzika Lukuvi

Familia Yashukuru Waliomzika Lukuvi

Familia ya aliyekuwa Mbunge wa Isimani na Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge, Sera na Wenye Ulemavu Marehemu William Vangimembe Lukuvi imetoa salamu za Shukrani kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha mazishi ya Lukuvi kitaifa ambayo yalifanyika kwa heshima kubwa.

Salamu za shukrani zimetolewa hii leo April 14, 2026 na familia ya Marehemu ikiongozwa na Mjane wa Marehemu Germina William Lukuvi ikiwa ni siku 14 zimepita tangu Lukuvi apumzishwe ambapo familia pia imeipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu chini Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba kwa kuratibiu kwa ufanisi Shughuli zote za Mazishi.

Aidha, familia imetoa shukrani za dhati kwa Viongozi wa Dini, wakiwemo Maaskofu na Mapadre, kwa kuongoza ibada za Misa Takatifu katika maeneo mbalimbali ikiwemo Dodoma, Dar es Salaam, Iringa Mjini na Idodi, Viongozi wa kimila wakiongozwa na Chifu wa Wahehe, pamoja na Mtwa Adam Sapi Mkwawa ametambuliwa mchango wao mkubwa wa Kimila katika kipindi cha msiba na mazishi ya marehemu.

Katika salamu hizo, familia imewashukuru Viongozi wa Chama na Serikali waliopo madarakani na wastaafu, akiwemo Makamu wa Rais, Rais wa Zanzibar, Rais Mstaafu Jakaya Msrisho Kikwete, Spika wa Bunge, Wabunge na Viongozi wengine wa Kitaifa na Mikoa kwa ushiriki wao, Pia familia imewashukuru Wananchi wa Jimbo la Isimani kwa namna ya kipekee kwa imani yao kwa Marehemu ambaye aliwatumikia kwa zaidi ya miaka 30 na familia imewahakikishia kuendeleza maono yake ya maendeleo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button