James Akamatwa Akijifanya Usalama

James Akamatwa Akijifanya Usalama

Jeshi la Polisi Mkoa wa Njombe limemkamata James Ngole (34) kwa tuhuma za kujifanya Afisa Usalama na kutumia kivuli hicho kutekeleza matukio ya utapeli kwa Wananchi wanaotafuta ajira.

Akizungumza kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga amesema Mtuhumiwa alikuwa akifanya mawasiliano na Watu mbalimbali katika maeneo tofauti ya Mkoani huo na kuwashawishi kuwa ana uwezo wa kuwapatia ajira Serikalini.

Kwa mujibu wa RPC Banga, Mtuhumiwa huyo alikuwa akiwataka waombaji kazi kutuma Vyeti vyao pamoja na fedha kwa madai ya kusaidia mchakato wa ajira. Hata hivyo, baadhi ya wahanga wamedai kupoteza fedha zao bila kupata ajira walizoahidiwa.

“Amekuwa akiwataka Watu watume Vyeti ili aweze kuwapatia ajira na baadhi ya wahanga wanadai kuchukuliwa fedha na hawajapata ajira, hivyo ni jambo la utapeli na huyu Mtu si Afisa wa Serikali,” amesema Banga.

Jeshi la Polisi limewataka Wananchi kuwa makini na Watu wanaojitambulisha kuwa Maafisa wa Serikali au wenye uwezo wa kutoa ajira kwa njia zisizo rasmi na kutoa taarifa kwa mamlaka husika wanapokutana na mazingira ya aina hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button