Mh. Anthony Mavunde (Mb) amewataka Wanazuoni kuwa sehemu ya upatikanaji wa suluhu ya utatuzi wa changamoto za kusaidia kuendeleza sekta ya madini

Waziri wa Madini, Mh. Anthony Mavunde (Mb) amewataka Wanazuoni kuwa sehemu ya upatikanaji wa suluhu ya utatuzi wa changamoto za kusaidia kuendeleza sekta ya madini ili iweze kukua zaidi na kuleta manufaa kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Ameyasema hayo leo tarehe 09 Juni, 2026 Jijini Dar es Salaam alipokuwa akifungua Wiki ya 11 ya Ubunifu na Utafiti iliyoandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Aidha, Waziri Mavunde amebainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi thabiti wa Mhe. Rais Dkt. Samia imeweka kipaumbele kwenye utafiti wa kina wa madini, ambapo kupitia Vision 2030 Madini ni Maisha na Utajiri tumejipanga kuhakikisha tunaongeza eneo lililofanyiwa utafiti wa kina kutoka asilimia 16 hadi asilimia 50 ifikapo mwaka 2030.

Vilevile, Mhe. Mavunde amepongeza programu ya Chuo kikuu cha Dar es salaam(UDSM) ya ubunifu na utafiti ambayo imewezesha vijana wengi kujiajiri na kusisitiza kwamba Vyuo Vikuu kupitia taaluma yao vinaweza kuwa ni kichocheo kikubwa cha ukuaji wa sekta ya madini kupitia tafiti zenye lengo la kutafuta suluhu za changamoto za sekta hiyo.

Awali, akitoa maelezo kuhusiana na Wiki ya 11 ya Ubunifu na Utafiti, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anayeshughulikia Utafiti, Prof. Nelson Boniface alibainisha kuwa maonesho hayo ni ya 11 kufanyika tangu walipoanza mwaka 2015 na yameweza kuibua mawazo bunifu mengi kwa wanafunzi yanayopelekea kujiajiri na kujipatia kipato pasipo kutegemea kuajiriwa.

Naye, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. William Anangisye ameeleza kuwa tangu kuanzishwa kwake, Wiki ya Ubuntu na Utafiti imeendelea kuchochea ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, Sekta binafsi kupitia wadau kama kampuni, taasisi za fedha na wadau wengine. Aidha, amebainisha kuwa kupitia kauli mbiu ya Mwaka huu wanataraji kuhakikisha taaluma inayozalishwa chuoni hapo inaingia kwenye sera na kupelekea matumizi ya teknolojia katika uvunaji wa rasilimali zetu kwa maslahi ya kizazi cha sasa na cha baadae

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button