Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amepuuza video iliyosambaa mtandaoni ikimuonyesha mkewe, Brigitte, akisukuma uso wake walipokuwa wakishuka kutoka kwenye ndege nchini Vietnam, katika awamu ya kwanza ya ziara yake Kusini Mashariki mwa Asia.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amepuuza video iliyosambaa mtandaoni ikimuonyesha mkewe, Brigitte, akisukuma uso wake walipokuwa wakishuka kutoka kwenye ndege nchini Vietnam, katika awamu ya kwanza ya ziara yake Kusini Mashariki mwa Asia.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Hanoi siku ya Jumatatu, Macron alizungumzia moja kwa moja kipande hicho cha video, akikanusha uvumi uliotokana nacho.
“Kuna video inayoonyesha nikifanya mzaha na kumtania mke wangu, na ghafla inageuzwa kuwa kama janga la kidunia, huku watu wakitunga hata nadharia mbalimbali kulieleza,” alisema rais huyo.
Macron alikiri kuwa video hiyo ni halisi lakini alikosoa jinsi ilivyotumiwa vibaya. “Video zote ni za kweli, na ndiyo, wakati mwingine watu huzihariri, lakini sasa watu wanaambatanisha kila aina ya upuuzi nazo.”
Kipande kifupi cha video kinaonyesha mlango wa ndege ukifunguliwa na Macron akionekana mlangoni. Sekunde chache baadaye, mikono yote miwili ya Brigitte Macron inaonekana ikimsukuma usoni kwa kile kinachoonekana kama msukumo wa ghafla.
Macron anaonekana kushangaa kwa muda mfupi lakini anajituliza haraka na kuwapungia waandishi wa habari waliokuwa nje.
Wanaposhuka ngazi za ndege, Macron anamtolea Brigitte mkono wake wa kumshika, lakini mke wake anakataa na badala yake anashikilia mpini wa ngazi.
Ikulu ya Élysée hapo awali ilikanusha kutokea kwa tukio hilo ndani ya ndege, kabla ya kujaribu kupunguza uzito wake.
Wenzi hao walikuwa wakibishana tu, kwa mujibu wa chanzo kilicho karibu na rais kilichoeleza kituo cha televisheni cha BFM TV, mshirika wa CNN. Ilikuwa ni “dakika ya kuwa pamoja,” kulingana na chanzo kutoka Élysée.
“Ilikuwa ni wakati ambapo rais na mke wake walikuwa wanapumzika kwa mara ya mwisho kabla ya kuanza safari, wakitaniana kwa utani,” chanzo hicho kiliiambia CNN siku ya Jumatatu.
“Hakuhitajika zaidi kuamsha mashine za waliobobea katika nadharia za njama,” chanzo hicho kiliongeza, kikisema kuwa watumiaji wa mtandao wanaounga mkono Urusi walilitumia tukio hilo kueneza mzozo bandia.
Macron amekuwa mstari wa mbele katika juhudi za kuratibu mwitikio wa pamoja wa Ulaya katika kuisaidia Ukraine kufuatia uvamizi wa Urusi mwaka 2022.
Tukio hilo mjini Hanoi linakuja wakati Macron anakumbana tena na wimbi la taarifa potofu mtandaoni. Mapema mwezi huu, Ikulu ya Élysée ilikanusha kama “habari za uongo” madai yaliyosambaa mitandaoni – na kuungwa mkono na maafisa wa Kremlin – kuwa Rais huyo wa Ufaransa alikuwa anatumia kokeini akiwa kwenye treni kuelekea Kyiv pamoja na Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer.
Uvumi huo, uliotokana na akaunti zinazounga mkono Urusi, ulidai kimakosa kuwa kitambaa kilichochanika ambacho Macron alikiokota kilikuwa mfuko wa kokeini. Ikulu ya Élysée ilijibu mtandaoni kwa kuandika: “Hiki ni kitambaa. Cha kupangusia pua… Umoja wa Ulaya ukianza kuwa kero kwa baadhi, taarifa za uongo hufanya kitambaa tu kuonekana kama dawa za kulevya.”
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Kremlin, Maria Zakharova, alichochea zaidi madai hayo, akidai kuwa tukio hilo lilikuwa sehemu ya matatizo makubwa ya bara la Ulaya. Maafisa wa Ufaransa walilaani kampeni hiyo kama sehemu ya juhudi zinazoendelea za Moscow kudhoofisha mshikamano wa Magharibi kuhusu Ukraine na kuathiri mazungumzo ya amani kwa kutumia simulizi potofu na udanganyifu wa mitandaoni.







