Sita Wakamatwa Mauaji Ya Polisi

Sita Wakamatwa Mauaji Ya Polisi

Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha linawashikilia Watu sita kwa tuhuma za mauaji ya Askari Polisi aitwaye Roland Mollel ambaye ni Mkazi wa Arusha yaliyotokea Aprili 15, 2026 muda wa usiku.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoani humo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Justine Masejo amesema kuwa tukio hilo lilitokea huko katika mtaa wa Mlimani, kata ya Muriet Jijini Arusha.

Aidha kamanda Masejo amebainisha kuwa Askari huyo wakati akiendelea na shughuli zake binafsi baada ya kazi, kulitokea taharuki iliyotokana na kusambaa maneno ya kundi la watu wakidai katika eneo lao kuna wezi wameonekana.

 

Ameendelea kufafanua kuwa wakati hayo yakiendelea, marehemu akiwa anapita na mtu mwingine ambaye inadaiwa ni dereva bodaboda wakiwa wamepakizana kwenye pikipiki, kundi hilo lilianza kuwashambulia huku wakiwakimbiza.

Aidha, amebainisha kuwa wanaendelea na msako wa kuwatafuta watuhumiwa wengine ambao wamehusika na pia wanakamilusha uchunguzi wa tukio hilo.

Jeshi la Polisi mkoani humo limetoa wito kwa baadhi ya wananchi wanaoendekeza tabia za kuchukua sheria mkononi kwa kuongozwa na mihemko kuacha kwani watambue wakifanya hivyo ni kuvunja sheria pamoja na kusababisha madhara kwa watu ambao hawana hatia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button