TRC yaongeza safari za SGR baada ya usumbufu kwa abiria

TRC yaongeza safari za SGR baada ya usumbufu kwa abiria

Shirika la Reli Tanzania (TRC) limeanzisha safari za ziada za Treni ya Reli ya Kisasa (SGR) kwa lengo la kuwahudumia abiria walioathirika na usumbufu wa safari uliotokea jana, Desemba 28, 2025.

Hatua hiyo imechukuliwa kufuatia maelezo ya Wizara ya Uchukuzi kuwa mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini zimesababisha athari katika miundombinu ya SGR na barabara, hali iliyoathiri ratiba za usafiri na kutishia usalama wa wasafiri.

Taarifa ya wizara hiyo kwa umma ilitolewa jana wakati huduma za SGR tayari zilikuwa zimeathirika, baada ya baadhi ya abiria kushindwa kuanza safari zao kwa mujibu wa ratiba.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, treni iliyopaswa kuondoka saa 12:00 asubuhi ilikwama katika Stesheni ya Magufuli jijini Dar es Salaam, na hadi saa 6:24 mchana haikuwa bado imeanza safari.

Wakati huo huo, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetangaza kuwa mvua zitaendelea kunyesha leo, Desemba 29, 2025, katika mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Mara, Simiyu, Rukwa, Songwe, Mbeya, Iringa, Njombe, Morogoro, Ruvuma, Lindi na Mtwara.

Akizungumza kupitia taarifa iliyotolewa kwa umma leo, Desemba 29, 2025, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano kwa Umma wa TRC, Fredy Mwanjala, amesema kuanzishwa kwa safari za ziada ni hatua ya kupunguza usumbufu uliowakumba abiria na kuhakikisha huduma zinaendelea kutolewa kwa ufanisi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button