Tume yataja maeneo yaliyoathirika zaidi kwa ghasia za Oktoba 29
Tume yataja maeneo yaliyoathirika zaidi kwa ghasia za Oktoba 29
Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, imebainisha kuwa ilifanya uchunguzi katika maeneo 202 yaliyoathirika zaidi, yakihusisha wilaya 21 kutoka mikoa 11 ya Tanzania Bara.
Akizungumza leo Alhamisi Aprili 23, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa kukabidhi ripoti kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji mstaafu Mohammed Chande amesema uchunguzi huo ulilenga kubaini chanzo cha matukio ya ghasia pamoja na kutoa mapendekezo ya namna ya kuimarisha amani nchini.
Ametaja maeneo yaliyoathirika zaidi ikiwemo Dar es Salaam, Mbeya, Songwe, Mwanza, Geita, Arusha, Iringa, Dodoma, Shinyanga, Ruvuma na Kimara.
“Uchunguzi ulihusisha maeneo 202 yaliyoathirika zaidi katika wilaya 21 na mikoa 11. Lengo lilikuwa kupata taswira halisi ya matukio na sababu zilizochangia uvunjifu wa amani,” amesema Jaji Chande.
Aidha, amesema tume hiyo ilitembelea pia Zanzibar na mkoa wa Kilimanjaro kama sampuli ya maeneo ambayo hayakukumbwa na ghasia, ili kujifunza mazingira yaliyosaidia kudumisha utulivu.




