WALIMU 3,153 WASHIRIKI SHINDANO LA STADI ZA UFUNDISHAJI

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetangaza kuwa jumla ya walimu 3,153 wamejisajili kushiriki Shindano la Taifa la Nne la Stadi za Ufundishaji kwa Walimu wa Shule za Awali na Msingi pamoja na Shindano la Pili la Stadi za Ufundishaji kwa Walimu wa Shule za Sekondari Tanzania Bara, hatua inayolenga kuimarisha ubora wa ufundishaji na ujifunzaji nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 2, 2026 jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir, amesema hafla ya utoaji wa zawadi kwa washindi wa mashindano hayo itafanyika Juni 6, 2026 katika Ukumbi wa Maktaba Mpya wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Mhe. Ameir amesema shindano hilo ni jukwaa linalowapa walimu fursa ya kuonesha umahiri, ubunifu na matumizi ya mbinu bora za ufundishaji darasani, huku likiwa sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Kitaifa wa Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini (MEWAKA).

Amesema kati ya walimu 3,153 waliosajiliwa kupitia Mfumo wa National Teaching Skills Competition System (TSCS), walimu 1,263 walikamilisha masharti yote ya ushiriki kwa kuwasilisha video za ufundishaji pamoja na maandalio ya masomo kwa ajili ya tathmini.

Mgeni rasmi katika hafla ya utoaji wa zawadi anatarajiwa kuwa Profesa Riziki Shemdoe, Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa huku mchakato wa tathmini ukiwa umekamilika na kupatikana kwa orodha teule ya walimu watano bora katika kila eneo la ushindani.

Mhe. Wanu amesema mshindi wa kwanza katika kila kundi atapata Shilingi milioni 2.5, cheti cha pongezi, cheti cha ushindi na kompyuta mpakato, huku shule anayofundisha ikipata projekta.

Aidha, shule zitakazotoa washindi wa kwanza katika maeneo ya Kusoma kwa Darasa la Awali, Kiingereza kwa Darasa la Kwanza na Ufaraguzi wa Zana kwa Darasa la Pili zitapatiwa vibao vya kielektroniki 100 vyenye thamani ya Shilingi milioni tano.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button