Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb) amejibu maswali kadhaa Bungeni leo Februari 7, 2024 jijini Dodoma,

Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb) amejibu maswali kadhaa Bungeni leo Februari 7, 2024 jijini Dodoma, kuhusu hatua na mikakati mbalimbali inayotekelezwa na Serikali katika kuimarisha Sekta ya Kilimo nchini.

Akijibu swali la Mbunge wa Sikonge, Mhe. Joseph Kakunda aliyetaka kufahamu ni lini mbolea ya ruzuku itaanza kuuzwa kwa bei elekezi inayozingatia ujazo wake, Waziri Bashe amesema kwa sasa mbolea ya ruzuku imeshaanza kusambazwa na kutoa agizo kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kuhakikisha kampuni za uuzaji wa mbolea zinafungasha mbolea kwa ujazo wa kilo tano, 10, 20 na kilo 50.

“Ninaagiza TFRA popote mlipo hakikisheni kuwa kunakuwa na vifungashio vya ujazo tofauti tofauti kuanzia kilo tano, 10, 20 na 50 na hakikisheni kuwa hata kwa wale wanaofunga kwa kilo labda iwe tano tano ikafika hata mifuko 10 yani ikawa kilo 50 bado bei yake ya uuzwaji haitakiwi kuzidisha thamani ya bei elekezi ya shilingi elfu sabini na tano kwa kilo 50,” amesema Waziri Bashe.

Ametumia pia wasaha huo kuziagiza kampuni za mbolea kuzingatia masharti ya uuzaji na kuepuka kuzidisha kiwango cha bei elekezi huku akitolea mfano wa kampuni iliyofungasha ujazo wa mifuko kumi ya kilo tano tano na kupata jumla ya kilo 50 ambapo iliuza mifuko hiyo ya kilo tano tano kwa Shilingi 13,000 kwa mfuko, hivyo kujikuta ikipata Shilingi 130,000.

Kuhusiana na changamoto ya wakulima wa Tumbaku kukosa bei ya Pembejeo mwaka 2023, Waziri Bashe amejibu kuwa kwa sasa Serikali inafanya kikokotoo kuona ni namna gani wakulima wa tumbaku wanapata ruzuku ya pembejeo na kuwahakikishia kuwa watanufaika na pembejeo kupitia mjumuiko wao wa wakulima wa Tumbaku.

Pia Waziri Bashe alijibu swali la Mbunge wa Kisesa- Mwanza, Mhe. Luaga Mpina aliyetaka kufahamu ni kwa kiasi gani Serikali imejipanga kukabiliana na changamoto za ugawaji wa ruzuku ya mbolea zilizojitokeza kwa msimu uliopita. “Kwa msimu huu changamoto kubwa ni kuwepo kwa baadhi ya wafanyabiashara wanaotaka kutorosha mbolea kwenda nje ya nchi, wameshindwa kuiba kwa kutoa takwimu hewa kwa kuwa huko kote tumebana,” ameeleza Waziri Bashe.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button