China Yaibua Vita Ya Kibiashara Dhidi ya Trump
China Yaibua Vita Ya Kibiashara Dhidi ya Trump
Baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kuanzisha utekelezaji wa amri ya kupandisha ushuru kwa bidhaa kutoka China, nchi hiyo imejibu kwa hatua za kisasi.
Taarifa iliyochapishwa na Ubalozi wa China nchini Marekani kwenye ukurasa wa X, ilidai kuwa, kile kinachofanywa na Marekani ni matokeo ya hasira zao kutokana na kuingizwa nchini humo kwa dawa za kutuliza maumivu makali aina ya Fentanyl zinazotoka China.
Marekani ilikosoa magenge ya dawa za kulevya kutoka Mexico kwa kusambaza Fentanyl, mwaka 2022 dawa hiyo ilisababisha vifo 109,680 nchini Marekani.
Katika taarifa hiyo, Ubalozi wa China ulisisitiza kuwa, Marekani inapaswa kufanya mashauriano ya usawa na China ili kutatua suala hilo.
“Ikiwa Marekani inataka kweli kutatua tatizo la Fentanyl, jambo sahihi ni kushauriana na China kwa kuheshimiana kama wenza sawa. Ikiwa Marekani inataka vita iwe ni vita vya ushuru, vita vya kibiashara au aina nyingine yoyote, tuko tayari kupambana hadi mwisho,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.