Waziri Kombo akutana na mwakilishi wa UNICEF
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo amekutana na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Bi. Elke Wisck kujadili kuimarisha ushirikiano katika kuwalinda watoto.
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam, Mhe. Kombo ameipongeza UNICEF kwa programu za watoto shuleni na kuwasihi kuleta wadau kutoka sekta binafsi ili kushirikiana katika programu za lishe shuleni na kuhimiza wazazi nchini kuzingatia lishe maalum za watoto chini ya miaka mitano zenye kujumuisha dagaa, mtama, uwele na ulezi pamoja na virutubisho vingine kwa watoto.
Aidha Mhe. Waziri Kombo amewasihi wazazi kuendelea kuwaelimisha mabinti umuhimu wa masomo kwao na kwamba wawe tayari kuwa mama pale wanapokuwa na uwezo wa kuwahudumia watoto wao wanaowaleta duniani.
Kwa upande wake Bi. Wisck akiongelea suala la lishe duni nchini amesema tatizo hilo lipo kwa wingi katika mikoa yenye kuzalisha mazao ya chakula kwa wingi.
Amesema kuwa kuna haja ya kuendelea kutoa elimu kwa wazazi hasa kina mama katika maeneo hayo ambao wengi wanajihusisha na kilimo na malezi ya watoto hao lakini hawazingatii milo ya watoto wanaowaacha nyumbani kwenda kwenye shughuli za kilimo.
Aidha, Bi. Wisck amemtaarifu Mhe. Waziri Kombo kuhusu ujio wa Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF ambaye atafanya ziara nchini wiki ijayo na kutembelea miradi mbalimbali ya UNICEF inayowagusa watoto wa kike.