Madai ya Katiba mpya, gharama za maisha zatajwa chanzo cha vurugu
Madai ya Katiba mpya, gharama za maisha zatajwa chanzo cha vurugu
Mwenyekiti wa Tume ya Kuchunguza matukio ya Oktoba 29, 2025 Jaji Mohamed Chande amesema maandamano ya vurugu zilizotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 wahusika walikuwa na malengo makuu matatu.
Akiwasilisha ripoti ya Tume hiyo kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan leo Alhamisi, Aprili 23, 2026 Jaji Chande amesema lengo la kwanza lilikuwa kuzuia uchaguzi usifanye na ndio sababu makundi ya waandamanaji walivamia kwenye vituo vya kupigia kura.
Amesema makundi hayo yalivamia na kuharibu vifaa vya kupigia kura, kushambulia askari polisi waliokuwa wakilinda kwenye maeneo hayo.
Kwa mujibu wa Jaji Chande lengo lingine lilikuwa ni kufikisha ujumbe kwa Serikali kutokana na changamoto ya gharama za maisha, uwepo wa demokrasia na haki sawa kwa vyama vya siasa pamoja na madai ya Katiba mpya.
Amesema kwa muda mrefu kumekuwepo kilio cha madai ya Katiba mpya hivyo, vurugu hizo zililenga kufikisha kilio hicho kwa Serikali na mamlaka husika.
Kwa mujibu wa Jaji Chande amesema baadhi ya makundi yalikuwa na lengo la kuvamia huku akieleza kuwa, wafanyabiashara waliofika mbele ya Tume walilalamika kuibiwa mali kwenye maeneo yao.
Oktoba 29, 2025 Tanzania ilikumbwa na vurugu kwenye maeneo mbalimbali nchini na kusababisha vifo, uharibifu wa miundombinu na mali za umma na watu binafsi.



