Polisi yamuita kada Chadema kutoa ushahidi madai mpango wa kumuua Lissu

Polisi yamuita kada Chadema kutoa ushahidi madai mpango wa kumuua Lissu

Jeshi la Polisi limesema linaendelea na uchunguzi wa kukusanya ushahidi wa taarifa ya Hilda Newton aliyoichapisha na kusambaza katika mitandao ya kijamii akidai Serikali kupanga kumuua Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Taifa, Tundu Lissu.

Wakati uchunguzi huo ukiendelea polisi imemtaka Hilda kufika ofisi ya mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai Dar es Salaam, kutoa ushahidi wa madai hayo, hata hivyo, mwenyewe amejibu kuwa anasubiria wito rasmi.

Taarifa iliyotolewa leo Jumatano Aprili 22, 2026 na Msemaji wa Polisi, David Misime inaeleza kuwa, Hilda alichapisha taarifa Aprili 10, 2026.

Kwa mujibu wa Misime, taarifa hiyo ya Hilda inaeleza kuwa, pamoja na mambo mengine Serikall imepanga kumuua Lissu (Mwenyekiti wa Chadema) kwa risasi.

“lli kukamilisha uchunguzi Jeshi la Polisi linamwelekeza Hilda kufika Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, iliyopo katika jengo la makao makuu ndogo ya polisi iliyopo Dar es Salaam Aprili 24, saa nne asubuhi ili kuwasilisha ushahidi aliosema na kuutangazia umma kuwa anao.

“Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 11 (2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2023,” amesema Misime katika taarifa hiyo.

Akizungumza na Mwananchi Hilda amesema,”nani alisema ushahidi unatolewa polisi? Kingine waniletee wito rasmi, wanajua pakunipata, si kipindi kile walivyonikamata walichukua details (vielelezo) zangu, wanajua pakunipata,” amesisitiza Hilda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button