RC MAKONDA AWATAKA WANAHABARI KUANDIKA HABARI ZA KULETA MABADILIKO CHANYA KWENYE JAMII
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Makonda, ametoa wito kwa waandishi wa habari kubadilika na kuandika habari zenye kujenga jamii badala ya zile zenye kuchochea migogoro au kueneza hofu.
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari yaliyofanyika leo katika Hoteli ya Gran Melia jijini Arusha, Mhe. Makonda amesema waandishi wa habari wana nafasi kubwa ya kuunda taswira na mwenendo wa jamii kupitia kazi zao.
“Waandishi wa habari wanaweza kuamua jamii iwe vipi kupitia kazi zao, kama vile mavazi, chakula na mwenendo wote wa maisha.” Amesema Mhe. Makonda mbele ya hadhira iliyojumuisha wanahabari, viongozi wa serikali na wadau wa sekta ya habari.
Aidha, Mhe. Makonda ametumia fursa hiyo kuwaalika wanahabari kushiriki kikamilifu kwenye jukwaa la kiuchumi7 litakalofanyika Mei 3, 2025, mkoani Arusha, akieleza kuwa hilo ni jukwaa muhimu kwa waandishi kupata taarifa sahihi na kuzifikisha kwa wananchi ili kuchochea maendeleo.
Maadhimisho hayo yamewakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya habari, huku ujumbe mkuu ukiwa ni kulinda na kuendeleza uhuru wa vyombo vya habari kwa maendeleo ya taifa.