Sehemu ya Pili : Kumuhusu SIMBAMANGU (Caracal )

SEHEMU YA 2.

Inaendelea toka post iliyopita nyuma

KUZALIANA
Paka hawa hubeba mimba kwa muda wa wiki 10 mpaka 11, ambapo ni kama miezi miwili na nusu na kuendelea na baada ya hapo huzaa watoto kuanzia 1 mpaka 4. Lakini kwa wastani huzaa watoto 2. Watoto hufungua macho baada ya siku moja japo wanaweza kuanza kuona vizuri mpaka wanapofikia siku ya 6 ama zaidi.

MAISHA YA UPWEKE
Paka hawa huwa hawatembei wala kuishi kwa makundi. Ni nadra sana utawakuta wapo wawili wameongozana isipokuwa inapofika wakati wa kuzaliana ndipo dume na jike wanaweza kukutana pamoja kwa ajili ya shughuli hiyo ya kutafuta familia.

HODARI WA KURUKA JUU
Paka huyu aitwaye simbamangu ni hodari sana wa kuruka ambapo anauwezo wa kuruka juu kwa kimo kinachofikia futi 10 (sawa na mita 3 ama zaidi). Hii humuwezesha kuvuka hata kuta na viunzi virefu ambavyo wanyama wengine hawawezi kufanya hivyo kabisa.

MIGUU YA NYUMA NI MIREFU KULIKO YA MBELE
Ukimtazama simbamangu akiwa kasimama, utamuona ni kama amebinuka kwenye kiuno na kuinamia mbele. Unaweza kumuangalia kwenye post ya kwanza picha yake na ukamuona vizuri.

UWINDAJI WA USIKU
Simbamangu ni jamii ya paka ambaye huwinda zaidi usiku kama ambavyo wafanyavyo paka wengine. Hawa ndo jamii ya wanyama ambao tunawaita kama nocturnal. Japo hata mchana anaweza kuwinda pia.

CHAKULA CHAKE NA VITOWEO
Simbamangu ni paka anayependelea kula wanyama wadogo wadogo na wakubwa kiasi ambao anajua anawamudu kupambana nao. Hula zaidi panya, sungura, pimbi, ngedere na swala wadogo kama digi digi, jamii za ndege na wengine wengi.

MAWASILIANO
Mawasiliano huwa ni kwa kutumia sauti ambapo mama na mtoto wanaweza kuwasiliana, ama dume na jike wanaweza kuwasiliana.

KUISHI MUDA MREFU BILA KUNYWA MAJI
Simbamangu pia huweza kuishi muda mrefu bila kuhitaji kunywa maji kutokana na maji anayoyapata kwenye vyakula anavyokula kila siku ambavyo ni nyama kwa wingi. Hana shida ya kunywa maji kila siku kama ng’ombe au mbuzi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button