Magumu Yaliyopo Kwenye Gereza Alilowekwa P Diddy
Magumu Yaliyopo Kwenye Gereza Alilowekwa P Diddy
Sean ‘Diddy’ Combs (54) ndiyo jina alilopewa na wazazi wake, lakini jina la kutafutia ugali
anajulikana kama P Diddy ama Diddy.
P Diddy ambaye ni msanii maarufu wa miondoko ya hip hop nchini Marekani amezuiwa katika gereza linaloitwa The Metropolitan Detention Center (MDC’ akikabiliwa na mashtaka ya uhalifu wa kingono.
Uamuzi wa kushikiliwa mahabusu kwa gwiji huyo wa muziki nchini humo ulitolewa na Hakimu wa Mahakama ya New York Robyn Tarnofsky baada ya kesi yake kusomwa Jumanne Septemba 17, mwaka huu na kukataa pendekezo la dhamana lililotolewa na mawakili wa Diddy.
Mwanamuziki huyo alishtakiwa kwa ulaghai wa kingono na usafirishaji wa binadamu ili kujihusisha na biashara hiyo ya ngono.
Mbali na hilo, waendesha mashtaka wanadai walikuta dawa za kulevya katika chumba cha hoteli alikokamatwa P Diddy Septemba 16, mwaka huu.
Akiwa mnahakamani P Diddy alikana mashtaka yanayomkabili na ombi la dhamana yake kugonga mwamba kisha kupelekwa mahabusu katika gereza hilo
maarufu kama The Metropolitan Detention Center (MDC)’.
Kwa mujibu wa Michael Cohen ambaye ni Mwanasheria wa zamani wa Mgombea Urais wa Republican, Donald Trump, gereza la The Metropolitan Detention Center (MDC)’ siyo tu sehemu ya ajabu, pia inatisha kwa msanii
huyo aliyezoea kuishi kwenye majumba ya kifahari yaliyopo katikati ya Jiji la Miami na Los Angeles nchini humo.
Cohen akizungumza na CNN amenukuliwa akisema; “Kila anapoamka anatazamana na kuta ngumu zilizonakshiwa rangi nyeupe zinazokinzana na aina ya ujenzi wa majumba yake ya kifahari,”
Akielezea sifa nyingine ya gereza hilo Cohen, alisema kwamba P Diddy anapaswa kufahamu kuwa amezuiwa katika moja ya magereza hatari zaidi ndani ya Jiji la New York, ndani ya gereza hilo ndipo mwanamuziki R. Kelly anapotumikia kifungo chake.
Mbali na Diddy na R. Kelly, wasanii wengine walioishia ndani ya gereza hilo ni pamoja na “Pharma Bro” Martin Shkreli, Mwanamitandao, Ghislaine Maxwell, mtaalamu wa biashara ya safari ya mtandaoni maarufu kama Cryptocurrency’ Sam Bankman-Fried na rapa Fetty Wap.