Operesheni ya kuwakamata waganga wa tiba asili na tiba mbadala wasio na leseni wanaojihusisha na ramli chonganishi zinazochangia vitendo vya ukatili dhidi ya watu wenye Ualbino.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Deogratius Ndejembi amewaagiza wakuu wa mikoa yote nchini kufanya operesheni ya kuwakamata waganga wa tiba asili na tiba mbadala wasio na leseni wanaojihusisha na ramli chonganishi zinazochangia vitendo vya ukatili dhidi ya watu wenye Ualbino.
Ndejembi ametoa agizo hilo akiwa mkoani Kagera wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kupinga ukatili dhidi ya watu wenye Ualbino iliyopewa jina la “Mimi Nipo na Mama Samia Suluhu Hassan, Ninapinga Ukatili Dhidi ya Watu Wenye Ualbino”.
Mbali na agizo hilo, Ndejembi pia amewataka wakuu hao wa mikoa kufanya kampeni ya kupinga ukatili dhidi ya watu wenye Ualbino katika halmashauri zote na kuhakikisha kamati za watu wenye ulemavu zinaimarishwa katika maeneo yao kwani ni takwa la kisheria kupitia sheria namba 19 ya mwaka 2010 wa watu wenye ulemavu.
“Pia ninatoa rai kwa wananchi wa mikoa yote nchini kuwa mabalozi wa ulinzi wa watu wenye Ualbino kwa kutoa elimu, kupinga ukatili na kutoa taarifa kwa viongzo pale wanaposikia ama kuona viashiria vya ukatili dhidi ya watu hao.” ameongeza Ndejembi






