Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Angola
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Angola, Mhe. Tete António, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Ziara ya Kitaifa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mazungumzo hayo, yamefanyika jijini Luanda, yamelenga kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya Tanzania na Angola, sambamba na kubadilishana uzoefu katika maeneo mbalimbali ya maendeleo ya kimataifa.
Aidha, viongozi hao wamejadili maandalizi ya ziara ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan inayotarajiwa kufanyika nchini humo tarehe 7- 9 Aprili 2025.
Viongozi hao pia wamesisitiza umuhimu wa ziara hiyo katika kuimarisha misingi ya ushirikiano kwa pande mbili hizo kwa maslahi ya wananchi wa Tanzania na Angola.