Diamond Atumia Story Ya Meek Mill Kufundisha Wachambuzi

Diamond Atumia Story Ya Meek Mill Kufundisha Wachambuzi

Diamond Platnumz ametumia mfano wa Meek Mill kama darasa kwa wachambuzi wa muziki Tanzania, akisisitiza umuhimu wa kuwa na uelewa mpana kuhusu mikataba ya muziki. Kupitia Insta Story yake, Diamond alichapisha taarifa inayoonesha jinsi MeekMill alivyoathirika kimapato licha ya kufanya kazi kwa zaidi ya miaka 13, akipata asilimia 13% tu ya mapato yake kabla ya kuwa msanii huru anayejitegemea na kumiliki kazi zake zote kwa asilimia 100%.

Diamond aliambatanisha taarifa hiyo na ujumbe mahsusi kwa wachambuzi wa muziki nchini, akieleza:

“Kuna somo kubwa hapa kwa wachambuzi wetu Tanzania kujua uhalisia wa biashara za label, zikioje ili kujua mtu anapokuwa yupo kwa mkataba wa kinyonyaji ama mkataba wa fair deal, inasaidia wakichambua wachambue kwa kusaidia na kujenga industry.”

Ujumbe huu unaibua mjadala mpana kuhusu maarifa ya wachambuzi wa muziki katika kuelewa aina za mikataba, iwe ya kinyonyaji au ya haki. Diamond anaamini kuwa kwa wachambuzi kuwa na taarifa sahihi, wataweza kuchambua kwa ufasaha na kutoa mchango chanya kwa ukuaji wa tasnia ya muziki.

Kwa mtazamo wangu kama mchambuzi, ni muhimu pia kwa lebo za muziki kuwa na uwazi katika baadhi ya vipengele vya mikataba, hasa vinavyogusa haki na maslahi ya wasanii. Mara nyingi wachambuzi wamekuwa wakitoa maoni kwa kutegemea taarifa zisizo kamili au za kusikia, na matokeo yake huwa ni lawama kwa lebo,na kumlinda msanii. Ikiwa lebo zitaweka wazi baadhi ya vipengele vya msingi kwenye mikataba yao, itasaidia kujenga taswira halisi ya mazingira ya kazi na kuondoa dhana ya unyonyaji.

Katika kipindi ambacho mjadala wa haki za wasanii na umiliki wa kazi zao unaendelea kushika kasi duniani, hatua ya Diamond inaweza kutazamwa kama wito wa mabadiliko kwenye mtazamo na uelewa wa wachambuzi wa muziki Tanzania, wito wa kuchambua kwa maarifa na sio uchambuzi wa kishabiki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button