NDEJEMBI AAGIZA MASHAMBA YA MAUA YA ROSE YALIYOSIMAMA ARUSHA KUREJEA KATIKA UZALISHAJI

  1. Makamau wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, ameagiza mashamba ya maua ya Rose yaliyosimama kufanya kazi jijini Arusha kurejea katika uzalishaji ili Tanzania iweze kunufaika tena na fursa za biashara ya maua katika masoko ya kimataifa.

Ndejembi ametoa agizo hilo leo Jumatatu Novemba 09, 2026, katika Viwanja vya TGT jijini Arusha, baada ya kufungua rasmi Maonesho ya Kimataifa ya Mbogamboga, Matunda na Maua ya HortiLogistica Africa 2026, akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amesema awali kulikuwa na mashamba yaliyokuwa yakizalisha maua ya rose kwa ajili ya kuuza nje ya nchi, huku baadhi ya mashamba hayo yakiwa na miundombinu ya uzalishaji na kusafirisha maua kwenda katika masoko ya kimataifa moja kwa moja kutoka Arusha.

Ameeleza kuwa ni muhimu mashamba yaliyobaki kurejea katika shughuli za uzalishaji zilizokuwa zikifanyika hapo awali ili Tanzania iweze kurejesha uzalishaji wa maua ya Rose yaliyokuwa na mahitaji katika soko la kimataifa na pita kutoa fursa za ajira kwa wananchi wa Tanzania hususan vijana.

Aidha, amewakaribisha wawekezaji kutoka duniani kote kutumia fursa zilizopo nchini katika sekta ya mazao ya bustani, ikiwemo uwekezaji katika uzalishaji, teknolojia bora, vituo vya kukusanyia mazao na miundombinu ya kuhifadhi bidhaa kupitia mifumo ya kisasa ya cold chain (miundombinu ya kuhifadhi na kusafirisha mazao katika mazingira yenye ubaridi unaodhibitiwa).

Amesema Serikali inatambua umuhimu wa sekta hiyo katika kukuza uchumi, kuongeza ajira na kipato cha wananchi, hivyo itaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuimarisha ushindani wa mazao ya Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button