TANZANIA NA ITU KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KUHARAKISHA MAGEUZI YA KIDIJITALI
Na Mwandishi Wetu, Geneva, Uswisi.
Tanzania imeahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano na Shirika la Kimataifa la Mawasiliano Duniani (ITU) ili kuharakisha mageuzi ya kidijitali kupitia upanuzi wa huduma za mawasiliano, usalama wa mtandao, ujumuishaji wa kidijitali na matumizi ya teknolojia zinazoibuka.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), alipokuwa akizungumza na Mkurugenzi wa Ofisi ya Maendeleo ya Mawasiliano ya ITU (BDT), Dkt. Cosmas Zavazava, jijini Geneva.
Mhe. Kairuki alisema Tanzania itaendelea kushirikiana na ITU katika kupanua intaneti ya kasi, kuongeza ujuzi wa kidijitali, matumizi ya Akili Unde (AI), kuimarisha usalama wa mtandao, huduma za serikali mtandao na mifumo ya tahadhari za mapema. Pia alieleza mafanikio ya Tanzania katika usalama wa mtandao, Kielelezo cha Maendeleo ya TEHAMA na uwekezaji wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.
Kwa upande wake, Dkt. Zavazava aliipongeza Tanzania kwa hatua zake za kuharakisha mageuzi ya kidijitali na kueleza kuwa ITU itaendelea kutoa utaalamu, kujenga uwezo wa wataalamu na kusaidia upatikanaji wa rasilimali. Alieleza pia kuwa programu za ITU, ikiwemo vituo vya mageuzi ya kidijitali na ubunifu, pamoja na mfumo wa serikali mtandao unaotumia Akili Unde na programu huria, zitasaidia kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za huduma za kidijitali.
Akihitimisha, Mhe. Kairuki aliishukuru ITU kwa ushirikiano wake na kueleza kuwa Tanzania ipo tayari kuwa mwenyeji wa vituo vya kikanda vya mafunzo ya kidijitali na kushirikisha mataifa mengine uzoefu wake katika utekelezaji wa miradi ya mageuzi ya kidijitali. Huku, Dkt. Zavazava akisisitiza umuhimu wa ujumuishaji wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika uchumi wa kidijitali






