#Yanga Haitaki Kufanya Makosa Dhidi ya #Rivers United


YANGA haitaki kufanya makosa katika mchezo wao wa ugenini dhidi ya Rivers United, hiyo ni baada ya kufanya umafia wakati leo Alhamisi kikosi hicho kikielekea Nigeria.

Wawakilishi hao wa Tanzania katika Kombe la Shirikisho Afrika, Jumapili hii watakuwa Nigeria kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Godswill Akpabio uliopo Akwa Ibom‎ katika Jiji la Uyo wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 30,000.

Msafarara wa Yanga, umepanga kuwapiga chenga wapinzani wao kwa kuamua kutofikia moja kwa moja katika mji ambao mechi itachezwa, na badala yake wataweka kituo Abuja.

Wakiwa huko, watatumia takribani siku mbili za maandalizi ya mchezo huo, huku malengo ni kutoruhusu mabao mengi, ili iwe rahisi kushinda nyumbani na kufuzu nusu fainali.

uelekea mchezo huo wa Jumapili, msafara wa watu 49 unaohusisha wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wa Yanga, alfajiri ya leo Alhamisi ulitarajiwa kuondoka kuelekea nchini Nigeria kupitia Ethiopia, huku wakitamba wanaenda kupambana kupata matokeo mazuri.

Akizungumza na Spoti Xtra, Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe, alisema: “Tunatarajia msafara wa watu 49 wataondoka nchini kesho (leo) saa 12 asubuhi kwa ajili ya mchezo wetu wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Rivers United utakaopigwa siku ya Jumapili.

“Tunaingia katika mchezo hu tukiwa tumetoka kupoteza mbele ya Simba, lakini jambo la muhimu ni kuwa hatukupata maeraha yoyote na wachezaji wote wana ari ya kuhakikisha tunapata matokeo, tunatarajia kuwa na progamu ya siku mbili ya mazoezi nchini Nigeria kabla ya mchezo.

“Beki wetu Mamadou Doumbia ambaye aliwekwa kwao Mali katika msiba wa baba yake, tutaungana naye tukifika Ethiopia, hivyo tunaenda tukiwa na kikosi kamili kwa ajili ya kupata matokeo mazuri.

“Ikitokea tumepoteza, lakini isiwe kwa mabao mengi, hiyo itatusaidia nyumbani kufanya vizuri na kutinga nusu fainali kwani tuna rekodi nzuri tukiwa nyumbani, ingawa ninaamini wachezaji wataifanya kazi yao vizuri, hatutapoteza.”

Yanga ambayo msimu huu ilianzia Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kuangukia Kombe la Shirikisho Afrika, katika michuano hiyo ya kimataifa msimu huu imecheza mechi sita Uwanja wa Mkapa, Dar, ikishinda mitano na sare mmoja. Haijapoteza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button