Zitto Afunguka Hukumu ya Rufaa ya Profesa Assad CAG Kichere
Zitto Afunguka Hukumu ya Rufaa ya Profesa Assad CAG Kichere
Kiongozi mstaafu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema uamuzi wa Mahakama ya Rufani uliothibitisha kuwa Profesa Mussa Assad aliondolewa katika wadhifa wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kinyume cha Katiba, umeimarisha ulinzi wa ofisi hiyo. Hata hivyo, Zitto ameeleza kusikitishwa na uamuzi wa Mahakama ya Rufani wa kutotoa nafuu kwa Profesa Assad, akisema ataendelea kuchukua hatua za kisheria kupigania suala hilo.
Zitto ametoa kauli hiyo kufuatia hukumu ya Mahakama ya Rufani liyokataa rufaa zote zilizowasilishwa na yeye na Serikali, huku ikithibitisha uamuzi wa Mahakama Kuu kuhusu kuondolewa kwa Profesa Assad. Amesema rufaa aliyokata ilikuwa sehemu ya jitihada za kulinda uhuru wa ofisi hiyo kwa mujibu wa Katiba. Hukumu hiyo ilitolewa Jumanne, Oktoba 6, 2026 na jopo la majaji watano wa Mahakama ya Rufani Barke Seheli, Lugano Mwandambo, Mary Levira, Panterine Kente na Mustafa Ismail. Profesa Assad aliteuliwa kuwa CAG Novemba 5, 2014 na alihudumu katika nafasi hiyo hadi Novemba 4, 2019, baada ya aliyekuwa Rais, Hayati John Magufuli, kumteua Charles Kichere kushika wadhifa huo.
Kufuatia hatua hiyo, Zitto alifungua kesi ya kikatiba katika Mahakama Kuu, Masjala Kuu Dar es Salaam, dhidi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Kichere na Profesa Assad. Katika Kesi hiyo ya Kikatiba Namba 8 ya mwaka 2020, Zitto alipinga kuondolewa kwa Profesa Assad kabla ya kufikisha umri wa kustaafu, akipinga pia uhalali wa kifungu cha 6(1) cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma Namba 11 ya mwaka 2008 kilichotumika katika kumwondoa.





