CCM na ACT Kufanya Maridhiano July 9
CCM na ACT Kufanya Maridhiano July 9
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi anatarajiwa kushuhudia hafla ya uwasilishaji wa Tamko la Pamoja la Maridhiano ya Kisiasa Zanzibar itakayofanyika Julai 9, 2026, saa nne asubuhi katika Ikulu, Zanzibar.
Tamko hilo linahusu muafaka wa kisiasa kati ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na ACT-Wazalendo ikiwa na lengo la kuimarisha maridhiano, mshikamano, utulivu wa kisiasa, amani na ustawi wa Zanzibar.
Katika hafla hiyo, Rais Dkt. Mwinyi pamoja na Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Taifa, Othman Masoud Othman watapokea uwasilishaji wa Tamko la Pamoja na kushuhudia utiaji saini wa ajenda zilizokubaliwa na pande zote mbili kwa ajili ya utekelezaji.
Hafla hiyo inatarajiwa kuhudhuriwa na Viongozi Wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Viongozi wa Vyama vya Siasa, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Viongozi wa dini, Wawakilishi wa Taasisi za kiraia pamoja na Waandishi wa Habari.





