Mahakama Yafuta Hati ya kumkamata Sativa na Kumrudisha Tanzania
Mahakama Yafuta Hati ya kumkamata Sativa na Kumrudisha Tanzania
Mahakama Kuu ya Tanzania imefuta hati ya kukamatwa na kurejeshwa nchini kwa mwanaharakati wa mtandaoni, Edger Edson Mwakabela, maarufu ‘Sativa255″, na kuitangaza amri hiyo kuwa batili. Uamuzi huo umetolewa Septemba 29, 2026 na Jaji Dafina Ndumbaro wa Kanda ya Dar es Salaam, baada ya kusikilizwa kwa rufaa ya Sativa aliyoiwasilisha kupinga amri hiyo iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Jaji amesema hati ya kukamatwa kwake na maelekezo ya kutumia njia zote kumrejesha Sativa, anayeishi Kenya (extradition), vimetangazwa kuwa batili, visivyo na nguvu na visivyo na athari yoyote kisheria. Kwa mujibu wa Jaji Ndumbaro, mwenendo wa shauri katika mahakama ya chini ulifanyika kinyume na kifungu cha 14(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), bila mamlaka ya kisheria chini ya Sheria ya Urejeshaji wa Watuhumiwa (Extradition Act), na kwa kutumia hati ya kiapo ya kuunga mkono shauri iliyokuwa na kasoro zisizoweza kurekebishika.
Sativa, kupitia wakili wake Jebra Kambole, alifungua rufaa dhidi ya uamuzi, mwenendo wa kesi na amri za Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu zilizotolewa Novemba 28, 2025, katika maombi ya jinai namba 28115 ya 2025.





