Mbinu Mpya ya usafirishaji Madawa ya Kulevya Kupitia Magari ya Maiti
Mbinu Mpya ya usafirishaji Madawa ya Kulevya Kutumia magari ya Maiti
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imesema baadhi ya magari yanayosafirisha maiti kwenda mikoa mbalimbali nchini yameanza kutumivwa na wafanyabiashara wa dawa za kulevya kusafirisha mirungi, bangi na skanka. Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas James Lyimo amesema hayo leo Jumanne, Septemba 29, 2026, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu operesheni zilizofanyika katika mikoa 14 kati ya Julai na Septemba 2026.
Mikoa hiyo ni Dar es Salaam, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Morogoro, Tabora, Shinyanga, Mwanza, Mara, Dodoma, Mbeya, Lindi, Mtwara na Ruvuma. Lyimo amesema taarifa za kiintelijensia zimebaini baadhi ya magari yanayosafirisha maiti kutoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya Kaskazini, ikiwamo Kilimanjaro, Arusha na Tanga kwenda kwenye misiba na kurejea ,yamekuwa yakitumiwa kusafirisha dawa za kulevya.
“Kwa mfano, magari yanayoenda ukanda wa Kaskazini, Moshi, Kilimanjaro, Arusha, Tanga na maeneo hayo, yanaporudi wakati mwingine yanabeba mirungi na mengine yanayoenda kule yanabeba skanka,” amesema. Amesema baadhi ya dawa hizo pia zimekuwa zikipelekwa katika maeneo inakofanyika misiba, huku mirungi ikiwa miongoni mwa dawa zinazotumiwa katika mazingira hayo.





